Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amewahakikishia wa Wasanii kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono wasanii wote na kuzitaka sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ziendelee kuwanufaisha vijana wengi zaidi hapa nchini.
Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo Novemba 11, 2022 wakati akizindua Tamasha la 41 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni linalofanyika katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) mkoani Pwani.
“Sanaa ndiyo roho ya taifa lolote pia hatuna budi kuhakikisha tuna Sanaa yenye asili na maadili yanayotuwakilisha sisi Watanzania, nawasihi Watanzania wenzangu na hasa wasanii wetu wa kizazi kipya kuepuka tabia ya kuiga kila tamaduni bila kuchuja wala kuzingatia maadili yetu” amesema Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango.
Makamu wa Rais ameongeza kuwa wasanii wanaweza kuiga yale mazuri yanayofaa na yanaendana na maadili ya Watanzania lakini yale yasiyotufaa tuwaachie wenyewe wenye tamaduni zao na ametoa rai kwa wasanii wa muziki na filamu kuhakikisha wanazingatia maadili na miongozo ya Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Bodi ya Filamu Tanzania kwa kutengeneza maudhui ya kazi zao na wakumbuke kuwa wasanii ni kioo cha jamii, wakitengezeza kazi mbaya jamii haitaheshimu kazi zao.
Halikadhalika Makamu wa Rais amewataka wasanii kutengeneza taswira nzuri katika jamii, walezi na wazazi ambayo haitawafanya wawe wagumu kuruhusu vijana wao kujihusisha na Sanaa kupitia muziki na filamu.
Mhe. Mpango ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo waendelee kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kuhifadhi, kutunza na kutangaza tamaduni za makabila yote ya Tanzania kupitia utalii wa kiutamaduni na kutoa nafasi kwa makabila yetu hapa nchini kuonesha tamaduni zake za chakula, dawa za asili, mavazi, makazi na aina za ngoma na burudani zake na kuongeza kuwa kila mkoa uweke utaratibu wake wa kuendeleza utamaduni wa mkoa husika iwe sehemu ya utalii wa kiutamaduni wa mkoa huo.
Aidha, ameelekeza kuwa Tamasha la Bagamoyo liendelee kuboreshwa kila mwaka ili lifikie hadhi ya matamasha mengine makubwa duniani. Wizara itoe kipaumbele katika kukitangaza Kiswahili duniani na kuanzisha kituo cha Sanaa cha watoto na vijana wenye vipaji na ambao hawapo kwenye mfumo rasmi wa elimu, kuanza ujenzi wa nyumba changamani na uzalishaji wa filamu na kuanzisha shule maalumu ya kukuza vipaji vya wanamichezo (sports Academy).
Mwisho Makamu wa Rais amesema Tamasha la Bagamoyo liendelee kuzingatia masuala ya Muungano kwa kuhakikisha vikundi vingi zaidi kutoka Zanzibar na sehemu zote za Tanzania Bara vinapata nafasi zaidi katika kushiriki Tamasha hili. Kwa kutekeleza maagizo hayo, wizara itapiga hatua kubwa sana na kubidhaisha Sanaa na Utamaduni wa mtanzania pamoja na kukuza Sekta ya Michezo nchini.
Kaole Road
Anuani ya posta: P.O.BOX 32 Bagamoyo Tanzania
Simu: +255 762544613
Simu ya kiganjani: +255 766 264 581
Barua pepe: application@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo yote yanayohusu masomo) info@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo ya ujumla) bagamoyofest@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo yote yanayohusu Tamasha) tas
Copyright ©2024 Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) . All rights reserved.