NI BAGAMOYO TENA
TAMASHA la 40 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), linatarajiwa kuanza Oktoba 28 hadi 30 mwaka huu, Bagamoyo, Mkoani Pwani.
Akizungumza mjini Bagamoyo, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Abdallah, amesema kuwa tamasha hilo linatarajia kushirikisha wasanii mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Aliwataka wasanii mbalimbali kuendelea kuthibitisha ushiriki wao katika tamasha hili ili kuhakikisha wanaendeleza sanaa ya muziki nchini.
Aliongeza, katika tamasha hilo wanatarajia ushiriki wa viongozi mbalimbali wa kitaifa, mabalozi, wakuu wa mikoa, wakuu wa Wilaya, wabunge, wakuu wa taasisi za serikali na sekta binafsi.
"Tamasha litarushwa mubashara na baadhi ya vyombo vya habari nchini, ili kuwapa fursa wananchi ambao hawatafika na kufuatilia wakiwa nyumbani.
“Litaonekana dunia nzima na hii inaitoa Bagamoyo na kuiweka katika ramani, Dunia na Tanzania waweze waweze kujua fursa zilizopo," alisema.
Alimshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abassi kwa kushirikiana na TaSUBa na Serikali ya Wilaya Bagamoyo kuhakikisha tamasha linafanyika kama lilivyopangwa.
Naye Mkuu wa TaSUBa, Dk. Herbert Makoye alisema tamasha hilo linabeba kaulimbiu isemayo, ‘Sanaa ni Ajira’ ikiwa ni mahsusi katika kuonyesha kuwa sanaa ni zaidi ya burudani, inaweza kuwa ajira au biashara na chanzo cha kipato kwa msanii.
Dkt. Makoye alisema tamasha hilo hufanyika kila mwaka na huandaliwa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) chini ya Wizara ya Sanaa Utamaduni na Michezo.
Alifafanua kuwa dhumuni la tamasha hilo ni kutunza na kuenzi sanaa na utamaduni wa Mtanzania, kutengeneza jukwaa ambalo wanafunzi wa TaSUBa wanalitumia kupima viwango vyao vya umahiri katika sanaa kwa mwaka katika fani za sanaa za maonyesho na zile za ufundi.
“Tamasha la mwaka huu litapambwa na ngoma za asili, muziki wa kizazi kipya, singeli, sarakasi, mazingaombwe, maigizo, maonyesho na biashara ya sanaa za ufundi,” alisema.
Dk. Makoye alisema jumla ya vikundi ambavyo vimethibitisha kushiriki mpaka sasa ni 70, ambapo vikundi vya ndani ya nchi ni 60 na vikundi 10 kutoka nje ya nchi.
Kaole Road
Anuani ya posta: P.O.BOX 32 Bagamoyo Tanzania
Simu: +255 762544613
Simu ya kiganjani: +255 766 264 581
Barua pepe: application@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo yote yanayohusu masomo) info@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo ya ujumla) bagamoyofest@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo yote yanayohusu Tamasha) tas
Copyright ©2024 Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) . All rights reserved.