Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kwa kushirikiana na Taasisi ya Bagamoyo Friendship Society ya Ujerumani imeendelea na kampeni yake ya kutoa elimu katika vijiji vya Msata na Msoga Wilayani Chalinze kuhusu athari za mimba za utotoni ambazo ni changamoto kubwa kwa ustawi wa mtoto wa kike.
Kampeni hii ambayo inafanyika katika baadhi ya Vijiji vya Wilaya za Bagamoyo na Chalinze imekua ya mafanikio makubwa kutokana na muitikio wa kuridhisha kutoka kwa wananchi kwa kuhudhiria kampeni hizo.
Kampeni imeanza Mei 06, 2022 na inafanyika kupitia sanaa shirikishi au sanaa kwa maendeleo ya jamii kwa mtindo wa igizo ambapo itadumu kwa muda wa kipindi cha wiki tatu.
Sanaa shirikishi ni tofauti na sanaa zingine za jukwaani ambazo zinakua ni za kufikirika tu. Sanaa shirikishi inaanza kwa hatua ya utafiti wa matatizo kwenye jamii husika, matatizo hayo yakibainika kutengenezewa sanaa kwa ajili ya kuielimisha jamii hiyo.
Aidha wananchi waliohudhuria kampeni hiyo baada ya igizo walipata fursa kupitia tafakuri ya sanaa waliyoiona kubainisha sababu za wasichana kupata ujauzito katika umri mdogo, changamoto zinazojitokeza baada ya mtoto kupata mimba na nini kifanyike ili kuepukana na changamoto hii.
Baadhi ya sababu za mimba za utotoni zilizotajwa ni mazingira magumu ya upataji wa elimu kwa mtoto wa kike mfano wanafunzi kutembea umbali mrefu kwenda shuleni, kuishi mtaani kutokana na ukosefu au upungufu wa hosteli, mila na desturi ya kuwacheza ngoma watoto wa kike kabla hawajamaliza shule, wahalifu kuendelea kuwepo mtaani kutokana na mashauri kumalizwa kienyeji, umaskini ambao huwafanya watoto wa kike waingie katika tamaa ya fedha, wazazi kutofuatilia maendeleo ya watoto shuleni, wasichana kutopata elimu ya jinsia na mahusiano, mmomonyoko wa maadili katika familia na jamii kwa ujumla.
Changamoto anazokutana nazo binti baada ya kupata ujauzito zilitajwa kuwa ni matatizo wakati wa kujifungua ambapo wakati mwingine hupelekea vifo kwa mama au/na mtoto, kufukuzwa nyumbani na wazazi, ongezeko la watoto wa mtaani, mtoto kushindwa kuendelea na masomo hivyo ndoto zake kukoma.
Wananchi hao walitoa suluhu kwa changamoto hizo kuwa ni pamoja na wazazi kuongea na watoto kuhusu mabadiliko ya miili yao, mabinti kutopewa uhuru uliopitiliza, elimu ya jinsia na mahusiano itolewe mashuleni, watoto wa kike wajengewe hosteli eneo la shuleni, sheria zisimamiwe kikamilifu, watekelezaji wa kadhia hiyo wapewe kifungo na adhabu kali, watoto wakishajifungua wapewe nafasi ya kurudi shuleni kumalizia masomo yao.
Mimba za utotoni imekuwa ni changamoto kubwa nchini, husani katika maeneo ya vijijini. Serikali ikishirikiana na wadau mbalimbali wa elimu, ustawi wa jamii, mashirika ya kitaifa na kimataifa inafanya jitihada kumkwamua mtoto wa kike katika changamoto hio kwa kuielimisha jamii wakiwemo wasichana wadogo mashuleni kuhusu athari za mimba hizo.
Kaole Road
Anuani ya posta: P.O.BOX 32 Bagamoyo Tanzania
Simu: +255 762544613
Simu ya kiganjani: +255 766 264 581
Barua pepe: application@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo yote yanayohusu masomo) info@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo ya ujumla) bagamoyofest@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo yote yanayohusu Tamasha) tas
Copyright ©2024 Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) . All rights reserved.