Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema Tamasha la 40 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni la Bagamoyo lililomalizika Oktoba 30, 2021 mjini Bagamoyo limetia fora kutokana na uratibu mzuri uliofanywa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo pamoja na wadau wengine.
Mhe Kikwete ameyasema hayo Oktoba 30, 2021 wakati akifunga Tamasha hilo ambapo amesisitiza kuwa limeunga mkono jitihada za Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan za kutangaza utamaduni wa Tanzania ambapo pia amepongeza kwa kushirikisha mataifa mbalimbali na kulifanya kuwa la kihistoria na kimataifa zaidi.
Amefafanua kwamba, hivi karibuni Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliandaa filamu ya Royal Tour iliyohusisha ziara kwenye mji wa Bagamoyo kwa ajili ya kutangaza utamaduni wa mtanzania.
Pia, amesifu uratibu wa siku ya mwisho la Tamasha la Kimataifa la Bagamoyo wa kuandaa ziara iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo Zainabu Abdallah, iliyoitwa jina la “Bagamoyo Royal Tour” iliyowajumuisha wasanii wa fani mbalimbali kama vile muziki, filamu, sanaa za ufundi, urembo na waandishi wa habari kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii katika mji wa Bagamoyo na baadaye mbuga ya Saadan.
Aidha, Mhe. Kikwete ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, kutumia Tamasha hili kwa kutoa huduma ya wachanjo ya Uviko -19 pamoja na kutoa ushauri na kupima UKIMWI kwa hiari.
Katika Tamasha hilo Mhe. Kikwete amefafanua umuhimu wa sekta hizi kwa Taifa letu ambapo amesema kutokana na umuhimu wa Sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo, haijawahi kutokea kuachwa kuundiwa Wizara katika awamu zote toka enzi ya Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Nyerere na kwamba kutokana na umuhimu huo Rais Samia ameendelea kuzibakiza na kuiziboresha.
Ameipongeza Wizara kwa kuendelea kuboresha sekta za Sanaa na Utamaduni kupitia taasisi zake za Bodi ya Filamu, COSOTA, BASATA na BAKITA na kuzitaka ziendelee kusimamia na kusaidia kazi za Wasanii ili waweze kunufaika nazo.
Aidha Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapa moyo Wizara kuendeleza Tamasha hilo lenye historia katika Taifa la Tanzania.
Amefafanua kuwa Tamasha hili ndiyo Tamasha kongwe zaidi nchini na limebeba historia ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo ambayo zamani ilikua ikijulikana kama Chuo cha Sanaa Bagamoyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuthamini mchango wa Tamasha hili ambapo ameahidi kuendelea kushirikiana na Wizara kuboresha Tamasha hilo ambalo amesisitiza kuwa lina faida kubwa siyo tu kwa wakazi wa Bagamoyo bali kwa taifa zima.
Kaole Road
Anuani ya posta: P.O.BOX 32 Bagamoyo Tanzania
Simu: +255 762544613
Simu ya kiganjani: +255 766 264 581
Barua pepe: application@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo yote yanayohusu masomo) info@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo ya ujumla) bagamoyofest@tasuba.ac.tz (Barua pepe hii inatumika kwenye mambo yote yanayohusu Tamasha) tas
Copyright ©2024 Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) . All rights reserved.